Header Ads

test

ODINGA AANIKA MITAMBO YA UCHAGUZI ILIVYODUKULIWA, KURA ZIKACHAKACHULIWA


Raila Odinga.
Mgombea Urais wa Muungano wa Upinzani (NASA), Raila Odinga amewaambia wanahabari kwamba wamepata habari kwamba mitambo ya Tume ya Uchaguzi (IEBC) ilidukuliwa na matokeo halisi yakachakachuliwa.

IEBC imekuwa ikitangaza matokeo ya awali ya urais mtandaoni, ambapo mpaka stori hii inapanda mtandaoni matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee akiwa mbele na kura 7,795,083 (54.38%) naye Bw Odinga akiwa na kura 6,433,161 (44.76%).

Bw Odinga, akiandamana na mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka na viongozi wengine wakuu wa NASA, amesema wadukuzi walitumia taarifa alizokuwa nazo meneja wa teknolojia wa IEBC Chris Msando aliyeuawa wiki moja iliyopita kuingia katika mitambo ya IEBC. Alienda mbele zaidi na kueleza kuwa baada ya kuingia, wadukuzi walitumia programu moja kuongeza matokeo ya Rais Kenyatta na kupunguza matokeo yake.

Amesema anaamini hilo lilifanyika katika kaunti zote na kwamba wagombea wa NASA katika nyadhifa nyingine, kura zao zimeharibiwa waliathirika pia. Hata hivyo, ametoa wito kwa wafuasi wa muungano huo waendelee kuwa watulivu.
Musyoka amesema anawashauri wafuasi wa muungano huo waendelee na shughuli zao za kawaida, ingawa huenda karibuni wakatakiwa kuchukua hatua. Odinga na Kalonzo wamekataa kusema ni hatua gani zaidi watachukua na badala yake wakasema wanasubiri kusikia ufafanuzi kutoka kwa IEBC kuhusu yaliyotokea.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati amewaambia wanahabari baadaye kwamba wamepata habari kuhusu tuhuma za muungano huo wa upinzani kwamba mitambo yao ya uchaguzi ilidukuliwa ambapo amesema tume haiwezi kupuuza tuhuma kama hizo na kwamba maafisa wake watafanya uchunguzi kubaini iwapo kuna ukweli wowote katika madai hayo.
Hata hivyo alieleza imani yake kwamba mfumo wa uchaguzi unaotumiwa na tume hiyo ni imara na kwamba ulitumiwa na shughuli zote za awali, na sasa “imesalia shughuli ya mwisho” ya kupeperusha na kutangaza matokeo ya kura.

Katika matokeo ya awali ya vituo 39091 kati ya 40883 yaliyopakiwa na IEBC mtandaoni:
  • Uhuru Kenyatta wa Jubilee ana kura 7,977,905 (54.32%)
  • Raila Odinga wa ODM ana kura 6,578,586 (44.79%)
Kura zilizoharibika kufikia sasa ni 387,959.

No comments